Udalali wa Nyumba na Viwanja: Mbinu 7 za Kupata Mafanikio

  | 4 min read
0
Comments
3641
udalali nyumba viwanja

Madalali wamerahisisha maisha ya watu wengi. Wamesaidia kuokoa muda na gharama kwa wengi wanaotafuta viwanja na nyumba za kupanga au kununua. Pia, kwa upande wa wamiliki wa nyumba na viwanja hivi, madalali wamekuwa daraja muhimu la kuwafikia wateja. 

Ili kufanikiwa katika biashara ya udalali wa nyumba na viwanja kunahitajika uvumilivu wa  kujifunza mambo mengi. Idadi kubwa ya madalali wanashindwa kazi hii katika miaka yao ya kwanza. Je unafanya nini ili kufanikiwa? Hizi ni baadhi ya dondoo muhimu za kufanikiwa katika biashara hii kutoka kwa madalali waliobobea na kufanikiwa katika biashara hii:

1. Kuwa Mvumilivu

udalali nyumba viwanja uvumilivu ndio nguzo

Biashara ya udalali inahitaji  uvumilivu mkubwa, hasa kwa madalali wapya wanaofanya kazi miongoni mwa madalali wenye uzoefu mkubwa wa kazi. Ili kuwa katika njia sahihi, dalali mpya lazima utambue na kuzitumia vyema fursa mpya zinazojitokea. Jaribu kuzungumza na madalali wenye idadi kubwa ya nyumba au viwanja vya kuuza au kukodisha. Pia, kumbuka fursa kama haijitokezi basi inabidi uitafute kwa namna yeyote ile. Ukipata wateja, hakikisha unakuwa na wakati wa makubaliano ili ujifunze na kuonesha  nia ya kufanya kazi kama dalali. Madalali wenye uzoefu wakikuamini kuwa unaweza kuwaletea wateja, basi itakuwa rahisi kukutafuta wakiwa na nyumba au kiwanja kingine. Na huo ndio utakuwa mwanzo wako mzuri.

2. Kuza Jina lako Mtandaoni

Jina ndio kila kitu siku hizi. Hasa ukiwa na jina linaloaminika miongoni mwa watu wanaotafuta nyumba na viwanja. Kama una kurasa za mitandao ya kijamii (mfano akaunti za Instagram, Facebook nk.), hakikisha unazitumia vyema. Jibu maswali  ya watu wanaouliza kuhusu vitu ulivyoposti. Hakikisha hakuna comments mbaya kwani wanunuzi hupenda kuangalia kama wanaweza kukuamini kabla ya kukutafuta kufanya biashara. Hakikisha kurasa zako za mitandao ya kijamii zinaakisi kazi unazofanya tu. Epuka kuchanganya posti zisizohusiana na kazi yako na posti za mambo ya  kisiasa au umbea wa mjini.  

3. Hakikisha Unapatikana na Mwenye Mawasiliano ya Haraka

nunua zoomtanzania wasiliana haraka

Ukiona mtu ametafuta hadi kupata kitu ulichokitangaza ujue ana shida nacho, hivyo ni muhimu sana kumjibu mapema. Usiweke tu namba ya simu halafu haijibiwi au haipatikani. Au unaposti kitu, watu wanakomenti kuuliza maswali na wewe unakuja kujibu  baada ya siku mbili. Hii ni hatari kwa biashara yako. Jibu haraka Ukishindwa kabisa, hakikisha kila mwisho wa siku umewasialina na mteja aliyekutafuta. Jiongezepale unapokuta ‘missed call’ kwa kupiga simu haraka — si unajua mteja ni mfalme? Kumbuka kwamba dalali hauko wewe mwnyewe, hivyo ukimkosa mteja, mshindani wako atampata. 

4. Kuwa Mwenyeji/Mwelewa wa Eneo Husika

Katika bishara ya udalali wa nyumba na viwanja, huwezi kufanikiwa kama hutajiongeza kujua eneo la biasharayako. Fikiria, mteja anatokea eneo fulani la mbali, anakuja kukutana na wewe kuhusu nyumba nzuri sana uliyoitangaza mtandaoni. Baada ya kuikagua anakuuliza — Shule ya karibu hapa ni wapi? Hujui. Hospitali iliyo karibu? Hujui. Wewe unajua tu bei ya hiyo nyumba au kiwanja. Hakikisha unakuwa na uelewa mzuri wa majirani na maeneo muhimu ya karibu. Vitu kama shule, hospitali, masoko na vituo vya magari au polisi ni muhimu kuwa katika listi yako. 

5. Mfanye Kila Mteja Kama Lulu

mpende mteja wako udalali nyumba viwanja

Hapa pia wengi wanasuasua hasa wakianza kufanikiwa. Usijaribu kamwe kubagua wateja kisa huyu amekufuata anataka bidhaa ya laki 5 na huyu anataka ya milioni 5. Wote hawa ni wateja wako, na ukimpuuzia moja kisa anachotaka kina thamani ndogo kidogo, kuna siku utamtafuta na kumkosa. 

6. Usiingie Nusu Nusu

Mwisho ni lazima kujitoa  kwa hali na mali ili kufanikiwa. Ili kufanikiwa katika kazi ya udalali, epuka sana kuingia nusu nusu. Asubuhi unazima simu ili ufanye kazi fulani, jioni unawasha ili ufanye kazi ya udalali. Kazi ya udalali sio kama ya Uber. Utakosa muda muhimu wa kuwasaidia wateja na watakukimbia. Ni muhimu kujitoa 100% ili upate muda wa kutafuta nyumba au kiwanja, kutafuta wateja na pia kuhangaika na hao wateja ili kuhakikisha wananunua au kukodi mali unayoitangaza. Ukishindwa kuwahudumia, wengine watawahudumia

7. Tengeneza Mtandao Wenye Nguvu

udalali nyumba viwanja tengeneza mtandao wa madalali

Madalali wengi wa nyumba na viwanja wana mtandao mkubwa unaowapa nguvu kwa wateja wao. Kuwa na koneksheni na madalali wengine ni muhimu. Dalali mwenye uwezo si tu yule anaekuwa na nyumba/kiwanja pale tu mteja atakapojitokeza. Bali ni yule ambae, hata mteja akija wakati hana hiyo nyumba basi ana uhakika wa kupiga simu kwa madalali wenzake na kupata suluhisho mara moja. Ni muhimu kuwa na mtandao unaowasiliana nao vyema mara kwa mara ili kujua walichonacho na wasichonacho. Kuna ushindani mkubwa kwenye soko, hivyo umoja wenye nguvu ni muhimu. Ili kufanikiwa usiingie kwenye biashara ya udalali wewe kama wewe, utashindwa. 

Mustapha Mosha
Mustapha Ally is a Community Marketing Manager at Zoom Tanzania and BrighterMonday Tanzania. He loves digital marketing social media