Njia 5 Rahisi za Kupata Uaminifu Kutoka Kwa Wateja Wako

  | 5 min read
0
Comments
2711
uaminifu wateja wapya

Fikiria umeingia katika mtandao au kurasa fulani wanayouza bidhaa mtandaoni. Hujawahi kuwasikia, lakini ukiangalia ubora wa bidhaa wanazouza unakuvutia sana. 

Kama ilivyo kwa wanunuzi wengi wa mtandaoni, utataka kuangalia ‘comments’ za wanunuzi wengine waliopita ili kujihakikishia kuwa biashara hiyo kweli ipo na watu wanafikiwa. Hii ndio njia ambayo wanunuzi wengi wamekuwa wakiitumia ili kuwaamini wauzaji wa bidhaa mtandaoni.

Sasa vipi kama biashara yako ni mpya? Mfano, ndio umefungua kurasa ya mtandao wa kijamii au webiste ya biashara yako. Hujawahi kuuza na hamna mtu aliyewahi kuacha ‘comment’. Je, utawezaje kupata uaminifu kutoka kwa wateja wapya? Hili ni tatizo ambalo karibu kila mjasiriamali mpya mtandaoni anakutana nalo.

“Imani ya mteja ni ngumu kuipata kama hujawahi kuwa na mteja”

Hivyo leo tutaangalia njia 5 rahisi unayoweza kutumia ili kupata imani ya wateja wapya na kuendelea kukua.

  1. Jenga Uhusiano Kupitia Maudhui

uaminifu wateja wapya

Maudhui ni njia muhimu ya kuungana na watumiaji wapya ambao hawajui wewe ni nani — hivyo unapata nafasi ya kujielezea polepole bila kuonekana unalazimisha kuwauzia. Mara nyingi kuandika makala kupitia blogu, hasa zile zinazoendana na bidhaa unazouza ni njia kuu. Hizi zitaonysha kiasi gani ulivyowekeza katika biashara yako, ulivyojikita kutatua matatizo ya wateja wako n.k kitu ambacho ndio wanachotaka kusikia kutoka kwako. 

Maudhui kama vile makala, video za kuelezea bidhaa, picha n.k, yanawafanya wateja waelewe kirahisi bidhaa zako, hasa kama utawaelezea jinsi inavyowasaidia huku ukiendelea kukuza jina lako. Hii itaonyesha ‘utu’ ulio nyuma ya bidhaa yako (unaonyesha unajali wateja zaidi), hivyo itakua rahisi wao kukuamini na kuamini biidhaa yako. 

Mfano, kama unafanya bishara ya kuuza magodoro, unaweza kuanza na kuandaa makala zinazoelezea umuhimu wa kupata usingizi mzuri usiku, na jisi ya kuupata usingizi huo.

Pia, hii inasaidiwa na wazo la kujadiliana na watu tofauti tofauti wanakaovutiwa na makala yako. Mfano, kama mtu aki ‘comment; katika makala uliyoiandika kuhusu bidhaa yako fulani, ni fursa kwako wewe kuweza kuongea nae na kuwa na uhusiano wa moja kwa moja.

2. Ainisha Sera Nzuri Inayowezesha Kuweza Kurudisha Bidhaa

Fikiria ndio unanunua bidhaa mtandaoni. Halafu wakati unataka kulipia, unaona sehmu imeandikwa ‘BIDHAA IKISHANUNULIWA HAIRUDISHWI WALA KUBADILISHWA’. Kama ujawahi kuwa na wateja watakaothibitisha kuwa bidhaa yako ina uhakika 100%, basi utafukuza wateja wote. 

Sera nzuri ya kurudisha bidhaa ni muhimu na ishara nzuri ya kuwajali wateja wako. Inaonyesha kwamba unawapa kipaumbele na kwamba unajiamini na bidhaa zako. Fikiria, mteja analipia lakini bado unamwambia, ‘Bidhaa ikisumbua au usiporidhika ndani ya siku 30, rudi nakubadilishia siku yeyote.’ Hii itajenga imani kubwa kwa wateja wapya na watakuwa tayari zaidi kununua kwa mara ya kwanza. 

3. Patikana Saa Zote Wateja Wakikutaka

uaminifu wateja wapya

Wateja ambao hawajawahi kununua bidhaa kwako na hawana uhakika na bidhaa zako wanaweza kukutafuta kwa njia tofauti. Hizi ni pamoja na fomu za kuwasiliana zilizo kwenye mtandao wako, Message za kwenye mitandao ya kijamii n.k. Wanaweza kutaka kujua unawatumia vipi mzigo kama wakinunua, wanarushaje kama bdhaa ikiwa haifanyi kazi, na taarifa nyingine za bidhaa. 

Ni muhimu sana kuwajibu haraka iwezekanavyo. We fikiria, nani ungemuamini zaidi? Kampuni inayotumia dakika 2 kukujibu swali lako kuhusu bidhaa unayotaka kununua au ile inayotumia siku nne kujibu? 

Katika kizazi hiki, spidi ya majibu kwa wateja ni muhimu sana. Unaweza ukaweka vitu kama ‘Chat’ za moja kwa moja katika tovuti yako, mitandao yako ya kijamii au hata namba za mitandao kama vile Whatsaap. 

4. Toa Maelezo ya Kina ya Bidhaa

Jinsi ambavyo wateja watajua zaidi kuhusu bidhaa unayoitangaza, ndivyo kuna uwezekano mkubwa zaidi ya wao kuinunua. Mfano, fikiria umetangaza simu unauza. Ukaandika tu ‘Samsung Galaxy’ inauzwa, Bei Poa njoo inbox’. Watu wengi wataishia hapo, kwanza wataogopa kabisa kutokana na maelezo nunu nusu ya bidhaa zako. 

Vitu muhimu vya kujumuisha wakati wa kuandika maelezo ya bidhaa yako ni pamoja na:

  • Vipimo sahihi vya bidhaa
  • Uzoto sahihi
  • Vilivyomo (Bidhaa imeunndwa na nini?)
  • Kuna ‘Waranty?’ Ni ya muda gani?
  • Kuna nini cha zaidi kuhusu bidhaa hivyo? Mfano, ‘Mikanda inayosogea kirahisi hivyo ni lazima nguo hii ikutoshe’ n.k

Ni muhimu pia kutumia picha na video nyingi ili kuelezea ubora wa bidhaa kwa undani sana. Hii itawasaidia wanunuzi kuweza kujiwekea picha kichani ya namna wanakavyojiona wakiwa wanatumia bidhaa yako. Hakikisha sana kuwa watakachokiona ndio watakachokipata.

5. Fikiria Kutoa Sampuli za Bidhaa Bure

uaminifu wateja wapya

Kupata wale wateja kadhaa wa mwanzo watakaokupa nafasi ya kukuamini na kukuwezesha kufungua macho ya wengine sio kazi ndogo. Njia moja ya uhakika ya kuhakikisha bidhaa yako inafika mikononi mwa wateja ni kuwapa sampuli za bidhaa bure. 

Kutoa sampuli za bure za bidhaa unazouza kunaweza kutengeneza wateja wa kudumu na uaminifu kwa wateja wako wapya. 

Japokuwa, kitendo cha kumpa mtteja bidhaa ‘ajaribu kabla ya kutumia’ si kwa kila bidhaa. Lakini kama unaudha bidhaa ambazo unaweza kumudu kutua sampuli kidogo (mfano tuseme unauza bidhaa ya chakula, unaweza kuwa na sampuli ya kuonjesha wateja kwanza). Mteja akionja/kujaribu ubora wa bidhaa yako na akafurahia, ni wazi utakuwa umeshinda moyo wake, hata kama hajawahi kusikia kwa mtu mwingine yeyote. 

Kuna njia kadhaa unaweza kutumia kugawa sampuli za bidhaa zako na bado kupata faida katika bishara yako changa:

  1. Kuwapa watu bidhaa ya bure watumie na kuwaomba watoe maoni yao kwenye bidhaa yako.
  2. Unaweza kutuma bidhaa kwa watu kadaa wenye ushawishi mtandaoni ambao wanaweza kusambaza neno zuri kwa watu wengi kuhusu bidhaa yako.
  3. Tembelea baadhi ya maeneo yenye mkusanyiko wa watu ambao huenda wakavutiwa na bidhaa zako. Mfano, eneo kama Mlimani City, Dar Free Market. Hawa ukiwagaia na wakapenda bidhaa yako, ni rahisi kuja kukutafuta baadae mtandaoni. 

Kumbuka kuwa, sampuli za bidhaa ni muhimu sana kutengeneza uaminifu kutoka kwa wateja wako. Hivyo ni muhimu kuhakikisha unaifikisha bidhaa kwenye mikono ya watu sahihi ili kurudisha thamani ya bidhaa ya bure unayoitoa.

Mustapha Mosha
Mustapha Ally is a Community Marketing Manager at Zoom Tanzania and BrighterMonday Tanzania. He loves digital marketing social media