Dondoo za Mahojiano ya Kazi ya Uyaya

  | 3 min read
0
Comments
4360
Mfanyakazi wa Ndani

Katika karne hii ya 21, wazazi hasa akina mama wanalazimika kufanya kazi ili kusaidia familia zao. Hivyo inakuwa ni muhimu kwa akina mama hawa kupata msaada hasa kama wana watoto. Mchakato mzima wa kufanya mahojiano ya kazi kwa ajili ya kupata mtu atakae kusaidia kuangalia watoto wako ni jambo gumu. Inabidi uhakikishe kuwa mtu unaye muajiri ni muadilifu maana atakuwa anakaa na watoto wako kwa muda  mwingi. Tumeandaa baadhi ya maswali yatakayokusaidia katika mahojiano hayo ya kutafuta yaya.

 

Anza na Mambo ya Msingi

Mjue mwombaji kazi kwanza, anza na salamu na maongezi ya utambulisho. Hii itamfanya mwombaji kazi atulie na aweze kujielezea vizuri. Unahitaji kujua historia yake vizuri kwa sababu atakuwa anahudumia watoto wako. Unaweza kuanza na:

 

Umekuwa unahudumia watoto kwa muda gani? AU  Umeshawaji kuwa yaya?

Watoto uliokua unahudumia walikuwa na umri gani?

Ungependa kuwa yaya kwa watoto wa rika gani? Na kwanini?

 

Utakaa Muda Mrefu na Familia?

Hili ni swali la muhimu, hasa katika jamii ya Watanzania. Mara nyingi yaya hukaa miezi michache na kisha huacha kazi, hii inawafanya wazazi wapate usumbufu wa kutafuta yaya mwingine ndani ya muda mdogo. Swali hili lita kuwezesha kujua uwajibikaji wa yaya huyo kwa familia yako. Pia kukaa kwa yaya muda mrefu kwenye kazi ni jambo zuri kwa wote. Kwani inatoa nafasi ya kuzoeana na kukuza uaminifu kati ya yaya na wazazi.

 

Maoni Yako Kuhusu Kuadabisha Mtoto Yakoje?

Adhabu kwa mtoto ni jambo nyeti sana. Hivyo kuuliza swali hili kutakuwezesha kujua ni jinsi gani yaya atamshughulikia mtoto wako pale anapofanya makosa. Mtoto anahitaji kujua pale anapofanya jambo zuri na pale anapofanya jambo baya. Unahitaji kujua kama namna ambavyo yaya atamuadhibu mwanao ni sahihi? Na umeridhika nayo? Au umuelekeze ni namna gani ungependa mtoto wako aadhibiwe. Kwa namna yoyote ile lazima mzazi na yaya wafikie makubaliano kabla ya kumshirikisha mtoto, kwani kumuadhibu mtoto pale anapofanya jambo baya ni vizuri kwa ajili ya kumkuza kiakili.

 

Muulize Kuhusu Unyanyasaji wa Watoto

Kumekuwa na matukio mbalimbali Tanzania ambapo yaya alikuwa akitesa watoto pale mzazi anapotoka kwenda kazini. Hii imetengeneza taswira mbaya kwa yaya wengi na imefanya wazazi wengi kukosa uaminifu kwa yaya. Kuuliza kuhusu suala hili kutakuwezesha kujua maoni ya mwombaji kuhusu unyanyasaji wa watoto, na upendo wao kwa watoto. Ni muhimu sana kujenga uaminifu kati yenu na kuelewana kuhusu namna ambavyo ungependa ashughulike na watoto wako.

 

Mahojiano kwa Vitendo

Kama sehemu ya mahojiano yako mpe muda, yaya ashughulike na watoto wako. Hii itakuwezesha kujua kama yaya anapatana na watoto wako, na kama anafaa kwa nafasi hiyo. Utakapokuwa umetoka utakuwa na amani ukijua watoto wako wanaangaliwa na yaya huyo? Utakapo mpa muda wa kushughulika na watoto wako chini ya uangalizi wako utaweza kulijibu swali hili kwa ujasiri.

Maswali ambayo hutakiwi kuuliza

 

Kuhusu Kabila lao
Kuhusu Dini yao
Kuhusu Mwelekeo wao wa Kijinsia
Kama wameolewa au wana mpango wa kupata ujauzito
Kuhusu Ulemavu wao

 

Elizabeth Nyimbo