Njia 3 Rahisi Za Kuongeza Wateja Wapya Katika Biashara Yako

  | 4 min read
0
Comments
16428
wateja wapya katika biashara

Ikiwa wewe ni mjasiriamali mchanga au mwenye uzoefu wa kuhudumia wateja hadi 10,000 — kamwe huwezi kuchoka kutafuta wateja wapya. Kwa wafanyabiashara wengi, mchakato wa kutafuta wateja wapya unaweza kuonekana kuwa mgumu na usiotabirika. 

Kama una ndoto za kukuza faida katika biashara yako inakulazimu  kuandaa mpango mkakati wa kuongeza wateja wako. Ni ngumu sana kuongeza thamani ya biashara yako kama miaka yote unahudumia idadi ile ile ya wateja. Ni lazima ufikiri namna nzuri itakayokuwezesha kupata wateja wapya na gharama za kuwafanya wafike dukani kwako. 

Mchakato wa kupata wateja wapya unajumuisha kutafuta watu na kuwashawishi ili waweze kuvutika na biashara yako. Baada ya hapo, wanaweza kufika dukani kwako kununua bidhaa hiyo au huduma.

Hizi ni hatua rahisi unazoweza kutumia kuwafikia watu wapya na kuwafanya kuwa wateja wa kudumu wa biashara yako.

 1. Tumia Matangazo ya Kulipia

matangazo ya kulipia

Moja ya njia ya haraka na rahisi ya kupata wateja wapya ni kupitia matangazo ya mtandaoni. Mitandao kama Facebook na Google wanaruhusu wafanyabiashara kuwafikia watu wapya ambao si wateja wao kwa kutumia matangazo ambayo gharama yake inaendana na bajeti ya mfanyabishara. Pia ni rahisi kupata taarifa muhimu za wateja wapya kama vile: maeneo walipo na muda gani wanakuwa wako mtandaoni. Pia unaweza kulipa gharama ndogo katika mitandao ya matangazo ya biashara kama ZoomTanzania ili tangazo lako lipate kipaumbele na kuonwa na watu wengi zaidi. 

Faida Zake

  • Biashara Inakuwa kwa kasi kubwa. Hii ni kutokana na idadi kubwa ya watumiaji wa mtandao huu ambao utaweza kuwafikia hata kama hawaijui bishara yako.
  • Unaweza Kulenga Kundi Maalum. Moja ya faida ya matangazo ya kulipia ni uwezo wake wa kukupa nafasi ya kuchagua nani aone tangazo lako au ni nani asilione. Mfano matangazo ya Facebook, unaweza kuchagua ni watu wa jinsia gani, umri gani, eneo gani au hata ni wenye kupendelea mambo gani ndio waweze kuona au wasione matangazo yako. 

Kasoro Zake

  • Inahitaji kujifunza. Kufanya matangazo ya kulipia hakuhitaji elimu ya chuo kikuu, bali inahitaji kusoma na kujifunza vitu muhimu vya kuzingatia ili kupata matokeo mazuri zaidi. Jambo zuri ni kwamba makampuni yanayotoa fursa za matangazo hayo kama Google na Facebook hutoa kozi bure.

2. Tumia Watu Wenye Ushawishi Mtandaoni (Influencers)

watu wenye ushawishi mtandaoni influencers

Kama una bajeti kidogo, moja ya njia za haraka za kuwafikia wateja wapya ni kupitia watu wenye ushawishi mkubwa mtandaoni. Hawa huwa na idadi kubwa ya wafuasi katika mitandao yao ya kijamii (Facebook, Instagram, Wamiliki wa Blog n.k). Hii imekuwa njia maarufu sana, hasa kwa biashara zinazochipukia. 

Ili ufanikiwe kupata matokeo mazuri, ni muhimu kupata mtu sahihi kwa ajili ya kutangaza bidhaa zako. Hapa, mtu sahihi ni yule mwenye wafuasi wanaoendana na aina ya bidhaa unazouza. Pia yule ambaye anaweza kusambaza tangazo la bidhaa yako  kwa namna ya kibunifu na itakayowavutia bila wafuasi wake kugundua anafanya tangazo. 

Faida Zake

  • Kukuza Jina la Bidhaa: Kutokana na watu hawa kuwa na maelfu au hata mamilioni ya wafuasi mtandaoni ni wazi kuwa ukifanya nao kazi wanaweza kukuletea wateja wengi na kukuza jina la bidhaa au huduma yako. Kwa mfano, fikiria umeamua kutangaza bidhaa yako ya kinywaji. Baada ya muda makundi ya watu tofauti wenye ushawishi na wafuasi wengi nchini Tanzania wanasambaza tangazo lako katika mitandao yao ya kijamii wakinywa kinywaji hicho na kuburudika. Kwa njia hii ni rahisi sana kuwahamasisha watu wengi na kukuza soko.

Kasoro Zake

  • Ni vigumu kujua nani ameleta wateja wangapi.

3. Andaa Orodha ya Barua Pepe

barua pepe kufanya biashara

Wakati mwingine, mteja anaweza kuona bidhaa unayouza kupitia kurasa za mitandao ya kijamii, tovuti au hata dukani mwako, lakini asitake kununua kwa wakati huo. Hivyo kuwa na barua pepe ya mteja ni njia mojawapo itakayokuwezesha kuwafikia kirahisi na kuwashawishi kununua bidhaa yako, labda kupitia punguzo kubwa la bei n.k. Tafiti iliyofanywa na Campaign Monitor inaonyesha kuwa, zaidi ya 595% ya wafanyabiashara wamerudisha fedha zao walizowekeza katika kampeni za kuuza kupitia barua pepe.

Unaweza kuandaa mpango wa kukusanya barua pepe za wateja wako. Mfano, kwa kuwa na kurasa maalum katika tovuti ya biashara yako ambapo endapo mteja ataacha barua pepe yake atapata punguzo la bei katika bidhaa fulani anayotaka kununua. 

Faida Zake

  • Kurudisha Mapato. Moja ya faida za kuuza kupitia barua pepe ni kwamba unakua na uhakika wa kumfikia mteja wako kwa kipindi kirefu. Hivyo ukimtumia vizuri ni rahisi kukuza thamani ya bidhaa zako.
  • Unakuwa na taarifa za mteja. Mbali na kumuuzia mteja bidhaa, pia barua pepe huweza kutumia kama njia ya kupata wateja wapya wanaofanana na mteja wako. Mitandao kama Facebook wanakupa mfanyabiashara nafasi ya kufikia wateja wapya kupitia matangazo, kwa kutumia orodha ya barua pepe utakazoziweka katika akauti yako hiyo. 

Kasoro Zake

  • Changamoto wakati wa kutuma barua pepe, kutokana na barua pepe nyingi kuishia katika ‘spam folder’ hasa kama barua pepe hizo hazikutumwa na mtu mwenye uzoefu wa kutosha.

Je, utatumia njia ipi kuongeza idadi ya wateja wapya katika biashara yako?

Mustapha Mosha
Mustapha Ally is a Community Marketing Manager at Zoom Tanzania and BrighterMonday Tanzania. He loves digital marketing social media