Njia 5 Salama za Kufanya Manunuzi Mtandaoni

  | 4 min read
0
Comments
2617
manunuzi salama mtandaoni

Manunuzi ya mtandaoni ni njia rahisi ya kuokoa muda na gharama. Badala ya kuchoma mafuta na kwenda kununua vitu, unafanya manunuzi yako kupitia simu ama  kompyuta. Lakini, kadri umaaarufu wake unavyoongezeka, pia ndivyo ambavyo hatari zake zinavyoongezea, kutokana na baadhi ya watu kujaribu kujinufaisha kwa kutapeli  wenzao . Wanaweza kuja kwa njia nyingi — kuna wale wanaowinda kadi zako za benki, wale wa miamala ya simu na hata wale wanaopanga kukuibia mtakapokutana ana kwa ana. 

Ripoti iliyopewa jina la ‘Economic Impact of Cybercrime, No Slowing Down’  iliyochapishwa na kampuni ya MacAfee inaonyesha kuwa mwaka 2018 pekee, gharama zilizosababishwa na wizi wa kimitandao ulifika hadi dola bilioni 600.

Hivyo basi, unafanya nini kuwa salama? Hakikisha hufanyi manunuzi mtandaoni bila kuzingatia dondoo hizi:

1. Fanya Manunuzi Katika Tovuti Salama Tu

fanya manunuzi salama mtandaoni katika tovuti salama

Kabla ya kuingiza taarifa zako za kadi ya benki au miamala ya simu, hakikisha umekagua kuwa tovuti unayoitumia kufanya manunuzi yako ni halali na ina ulinzi. Njia rahisi ya kutambua hili ni kwa kuangalia alama ya ‘https’ mwanzo wa anuani ya tovuti hiyo. Kama hiyo tovuti haina alama ya ‘s’ baada ya ‘http’ basi jua kuwa tovuti hiyo haijahakikiwa na si salama kuingiza taarifa za miamala yako ya kifedha. Tovuti za mitandao yote lazima iwe na ‘s’, kifupi cha neno ‘secured’ mwishoni mwa anuani ya tovuti hiyo. Mfano tazama namna ya tovuti salama na ambayo sio salama itakavyoonekana.

  • https://www.jinalatovuti.com (tovuti hii ni salama)
  • http://www.jinalatovuti.com (tovuti hii si salama). Haina ‘s’ baada ya neno http

2. Mfahamu Muuzaji na Hadhi Yake

Kama tayari unafahamu duka la bidhaa unazozipenda, basi kufanya malipo katika tovuti yao ili kununulia mtandaoni sio shida sana. Ni rahisi kwenda moja kwa moja katika duka lao endapo shida yeyote itatokea. Mfano, unajua kabisa duka fulani la kuuza saa lipo Mlimani City, na pia wana website inayotambulika. Hivyo unaweza kufanya malipo mtandaoni kwa uhakika kwani unajua kabisa lolote likiwa ndivyo sivyo basi ni rahisi kwenda kuripoti dukani kwao.

Kama hufahamu duka lao, basi bado huo sio mwisho wa kufanya manunuzi — unahitaji tu kuchukua tahadhari za ziada. Fanya tafiti ndogo kwa kuangalia maoni ya watumiaji wengine wa mtandao huo. Ikiwa wengi wanatoa maoni hasi, au hakuna maoni kabisa basi chukua tahadhari wakati wa kufanya malipo huko.

3. Epuka Kutumia Internet ya Umma (Public Wi-Fi) Kufanya Manunuzi

Fanya manunuzi salama mtandaoni epuka free wifi

Wote tunazijua hizi. Unafika sehemu, mfano Viwanja vya Ndege au baadhi ya Migahawa. Unakuta wameweka alama ya ‘Free Wi-Fi’ au ‘Internet ya Bure Hapa’. Hizi zinakua sawa kama unaperuzi mtandaoni au kuangalia video. Lakini si salama kuingiza nyaraka zako za siri mfano taarifa za kifedha. Mara zote unapoingiza taarifa binafsi katika ‘Internet za bure’ basi unafungua mlango kwa wezi wa mtandaoni. Intaneti nyingi za bure huwa hazijaandaliwa kulinda taarifa zako (unencrypted), hivyo wezi wanaweza kukuibia kirahisi ikiwa watajiunga kwenye Internet ya bure kama wewe. 

Kama unahisi umeperuzi na kupenda kitu, basi subiri hadi ufike nyumbani kwenye internet yako salama, au tumia internet ya simu yako. Inaweza kuwa iko polepole, lakini ni salama zaidi. 

4. Usitumie Neno Siri Moja na Badilisha Mara kwa Mara

Tunajua kuwa inachosha sana kubadilisha ‘passwords’ mara kwa mara kwenye sehemu zote ulizoingiza taarifa zako. Shida inakuja pia kuzikumbuka kila mara utakapotaka kuingia. Lakini kama kweli unataka kuweka taarifa zako salama (hasa za miamala ya kifedha) wakati wa kufanya manunuzi mtandaoni, basi ni muhimu kutokutumia ‘pasword’ moja katika akauti zako zote. We fikira, mdukuzi anafanikiwa kudukua neno siri lako la Facebook, na ndio hilo hilo umetumia Benki, mitandao ya malipo kama Paypal, Email zako n.k, utapona kweli? Pia hakikisha kuwa unabadili neno la siri la akaunti hizo kila baada ya muda fulani

5. Kuwa Mjanja Dhidi ya Apps za Manunuzi

fanya mnunuzi salama mtandaoni kuwa mjanja dhidi ya app

Apps za manunuzi zinafanya mambo kuwa rahisi sana, ikiwemo pia kuibiwa. Ukiwa na App, unapata urahisi wa kuperuzi na kufanya maamuzi ya kulipia n.k. Lakini pia, App zinatengenezwa kwa namna ambao ni rahisi kuiba taarifa zako na za kwenye simu yako. Mara zote hakikisha unapakua (download) App zako kutoka katika vyanzo vya kuaminika, mfano Google PlayStore na Apple App Store. Weka umakini pia wakati wa kuruhusu App hiyo kufanya baadhi ya vitu. Kama ukiona kitu hakileti maana, mfano App inaomba ku’access’ orodha ya namba zako za simu, lazima uwe makini. . Pia soma maoni (reviews) yanayotolea na  watumiaji wengine kabla ya kuhifadhi App hiyo katika simu yako.

Mustapha Mosha
Mustapha Ally is a Community Marketing Manager at Zoom Tanzania and BrighterMonday Tanzania. He loves digital marketing social media