Malengo ya Mwaka Mpya: Njia 5 za Kuanza Mwaka Wako Vyema

  | 3 min read
0
Comments
2833
malengo ya mwaka mpya

Mwaka mpya unatupa mwazo mpya na nafasi ya kutafakari mipango ya mwaka jana na namna ya kujiandaa na mwaka ulio mbele yetu. Ni vema Kuweka malengo na namna ambavyo utaweza kuyafikia mapema, hasa kipindi kama hiki cha Januari. Sio kazi ngumu. Unaweza ukachukua muda mchache tu na kuandika malengo utakayotaka kukamilisha mwaka huu. Hizi ni namna ambavyo unaweza ukajiwekea malengo bora zaidi kwa mwaka huu:

1. Tafakari Kuhusu Mwaka Ulioisha

malengo ya mwaka mpya tafakari mwaka wako

Kabla ya kuanza kupanga mipango ya mwaka huu, ni vyema ukaangalia  ulipotoka kwanza. Kuna uwezekano mkubwa ukahitaji kuazima baadhi ya mbinu ulizotumia  kukamilisha malengo fulani mwaka jana. Pia, itakupa nafasi ya kujifunza kutokana na mipango ambayo haikwenda kama ilivyotakiwa mwaka jana. Unaweza kujiuliza maswali machache kama;

  • Wapi nilitumia hela na muda mwingi sana mwaka jana?
  • Tabia gani nahitaji kuachana nazo?
  • Ni jambo gani zuri nilifanikisha mwaka jana? Na kadhalika.

Maswali kama haya yatakupa mawazo yatakayokusaidia kuweka malengo mazuri zaidi kwa mwaka huu

2. Malizia Ulivyoviacha Mwaka Jana

Ni mipango ipi au kazi zipi  ambazo ulipanga kuzikamilisha mwaka jana na hukufanikiwa? Unaweza kuikamilisha kabla ya kuanza mipango mipya ya mwaka huu? Kuna uwezekano ya kuijumuisha mipango ya mwaka jana katika mipango ya mwaka huu ili uifanyiekazi pamoja? Kwa namna yeyote ile, usiache mipango ya mwaka jana ambayo hukuikamilisha iende na maji. Usikubali akili yako izoee kutokamilisha/kushindwa  vitu. Tafuta namna ya kumalizia mipango yako kwanza na hapo ndio utaweza kuianza vyema ya mwaka huu.

3. Weka Mkazo kwenye Malengo Yenye Uhalisia

malengo ya mwaka mpya

Sawa, tunashauriwa tuwe na ndoto kubwa. Lakini kiukweli huwezi ukajiwekea malengo makubwa ambayo huwezi kuyatimiza. Utakua unajitengenezea mazingira ya kujiona unashindwa. Kama unahitaji kukamilisha mipango yako ya mwaka huu vyema basi iwe yenye  uhalisia. Weka malengo ambayo utaweza kutengeneza picha kichwani ya jinsi utakavyoyatimiza.

4. Usisahau Afya Yako Mwaka Huu

Bila kujali majukumu, malengo au umri, kamwe usiache kujali  afya yako kwenye malengo yako ya mwaka huu. Fikiria kama utaweka mipango mingi mizuri kisha kushindwa kuitimiza kwa sababu ya magonjwa ambayo ungeweza kuyaepuka. Zipo namna nyingi apazo unaweza kuchagua ili kuishi maisha yenye afya bora mwaka mzima. Mfano:-

  • Kujiwekea ratiba nzuri ya kupata muda wa kutosha kupumzika. Huwezi kutimiza malengo yako ukiwa umechoka choka.
  • Kujijengea mahusiano mazuri ya kijamii.
  • Kufanya mazoezi ya kutosha. Na sio lazima uende Gym. Unaweza kujinunulia vifaa vya kufanyia mazoezi nyumbani na bado ukawa fiti mwaka mzima
  • Kujiwekea ratiba ya kumwona Daktari mara kwa mara.

5. Jifanye Uwe Kipaumbele Chako Mwaka Huu

malengo ya mwaka mpya jipe kipaumbele

Umewahi kusika ule msemo kwamba ‘huwezi kuwasaidia wengine mpaka uweze kujisaidia mwenyewe kwanza?’. Hiki ndicho hasa unatakiwa kukifanya mwaka huu kama utahitaji mafanikio. Hii haimaanishi kwamba hutakiwi kuwasaidia wengine, hapana. Cha kufanya ni kuhakikisha kwamba unatenga muda mzuri wa kukamilisha malengo yako na unautumia muda huo kufanya hivyo. Ukifanikisha malengo yako vyema, ni wazi kabisa itakua rahisi watu wengine kukupenda kutokana na mafanikio yako.

Umepanga vipi kuanza mwaka wako? Tuambie mawazo yako kupitia sehemu ya comment hapo chini.

Mustapha Mosha
Mustapha Ally is a Community Marketing Manager at Zoom Tanzania and BrighterMonday Tanzania. He loves digital marketing social media