Makosa 5 Wafanyayo Wengi Wakati wa Kupanga Nyumba

  | 4 min read
0
Comments
7970
nyumba kupanga makosa

Kupanga nyumba ni hatua muhimu katika maisha. Inahitaji umakini na muda wa kutosha kwani ukikosea, basi inaweza kukugharimu muda, nguvu na hata furaha katika kipindi fulani. Na kama tunavyojua, wamiliki wengi wa nyumba hupendelea kuchukua kodi ya jumla ya kipindi fulani (miezi 3, 6 au mwaka) ili kuepuka usumbufu wa wapangaji wao. Hivyo kuna makosa ambayo huna budi kuyaepuka wakati unapanga nyumba au sehemu ya nyumba (apartment au chumba), kwani ukikosea, utajuta ndani ya miezi 3, 6 au hata mwaka. 

Haya ni baadhi ya makosa wanayofanya watu wengi na kuishia kuishi maisha wasioyategemea kwa kipindi kirefu mpaka hapo kodi itakapoisha.

1. Kusaini Mkataba Wa Nyumba Bila Kuusoma 

nyumba kupanga makosa

Hijalishi uko makini kiasi gani, makosa yanaweza kutokea. Kama ilivyo kwa namna ambavyo watu wengi hupuuzia kusoma vigezo na masharti vya matumizi ya bidhaa mbali mbali, basi wengine hufika mbali zaidi hadi kwenye mikataba ya nyumba.

Ukweli ni kwamba, watu wengi hawaoni umuhimu wa kusoma mikataba. Wengi wanaona ni makubaliano tu ya kisheria kati ya mwenye nyumba na mpangaji wake, lakini mara nyingi huwa ni kanuni na sheria za mwenye nyumba kwa mpangaji wake. Hivyo, kusoma mkataba wako ni lazima. Usipuuzie kitu utakachokuja kujutia mwaka mzima. 

2. Kupuuzia Mazingira ya Nje

Wakati mwingine, unaweza kuwa kwenye haraka sana ya kupata nyumba ya kupanga. Hivyo ukaamua kulipa haraka nyumba uliyoonyeshwa mara moja kabla mwingine hajailipia. Unapuuzia mazingira yanayozunguka nyumba yako kama majirani, mwonekano, usalama n.k. Baada ya kuhamia, ndipo majuto yanakuja kufuata. Usikubali haja ya kupata nyumba kwa haraka ikufanye usiliangalie hili. Unaweza kuangalia nyumba mara ya kwanza, na kesho yake kuja kuikagua mazingira ya nje ili kuhakikisha ni salama na kama unavyotaka. Kuna nyumba ambazo, asubuhi pamepoa na pako kimya sana, lakini jioni mazingira ni kelele kuliko kawaida, huwezi kulala. Pia, unaweza ukaangalia vitu kama umbali wa soko, hospitali shule n.k. Ni muhimu sana kwani ukikosea hapa pia, utajutia kwa muda mrefu. 

3. Kupangisha Nyumba Bila Kuiona Kwa Macho

nyumba kupanga makosa

Kwa teknolojia ilipofikia, hakuna ubaya wowote kupitia nyumba za kupanga mtandaoni wakati unatafuta nyumba ya kupanga. Kosa linakuja pale unapoona picha za nyumba na ukaipenda, na kwa hofu ya kuikosa ukaamua kuilipia (au kufanya malipo nusu) kabla haijawahiwa. Sababu kubwa tu ni kuwa, umeona imeandikwa ina chumba kikubwa na sebule yenye marumaru ya kuvutia, na ipo karibu na barabara (kama madalali wengi wanavyoandika ili kurembesha biashara zako. Kama tulivyosema pointi ya juu hapo, ni muhimu kuikagua nyumba kwa macho yako, ndani na nje kwa majirani. Na kama ukiweza nenda urudi siku inayofuata kuhakikisha umeona unachotaka. Ni bora uikose nyumba hiyo kwa kuchelewa kulipa, kuliko kulipa na kuja kujuta kwa miezi sita au mwaka mzima. 

4. Kuacha Kurekodi Sehemu Mbovu Kabla ya Kuhamia

Kabla ya kuhamia, ni muhimu kuwa na kumbukumbu (picha au makubaliano na mwenye nyumba) ya nini kibovu kabla ya kuhamia. Unaweza kukuta nyumba ilikua na ufa kabla hujahamia lakini mwenye nyumba hakuuona. Hivyo siku za mbeleni akiuona anaweza kusema wewe unahusika moja kwa moja na ufa huo. Hivyo, ni muhimu sana kupicha picha, au kuomba kurekebishiwa sehemu yeyote yenye kasoro kabla ya kuhamia. Unaweza ukatoa nakala ya picha na maelezo kumpa mwenye nyumba ili awe anajua uwepo wa tatizo hilo na kwamba na wewe unalijua kabla haijahamia. 

5. Kushindwa Kutoa Taarifa Kuhusu Ubovu wa Nyumba

nyumba kupangisha

Hii pia inaweza kuwa mwendelezo wa pointi ya hapo juu. Sio tu unatakiwa ukiona ubovu wa nyumba basi uishie kupiga picha, bali ni lazima kutoa taarifa za ubovu au uharibifu mapema iwezekanavyo. Mfano fikiria, unaweza kupuuzia tundu dogo la sinki la jikoni linalodondosha maji wakati wa kuosha vyombo. Bila kujua, ukubwa wa tatizo unaweza kuongezeka kwa kuozesha mbao, au kusababisha shoti ya umeme na kufanya mambo kuwa makubwa kuliko mwanzo. Kama unadhani unaweza kurekebisha baadhi ya vitu basi ni vyema kufanya hivyo mapema. Usisubiri mambo yameharibika ndio utoe taarifa, utalipishwa.

Mustapha Mosha
Mustapha Ally is a Community Marketing Manager at Zoom Tanzania and BrighterMonday Tanzania. He loves digital marketing social media