Hatua 3 Rahisi za Kuuza Nyumba Kwa Haraka na Kupata Faida

  | 4 min read
0
Comments
3324
kuuza nyumba

Ukifika wakati umeamua kuhamia nyumba nyingine, mkoa au nchi, au pengine unataka pesa kwa sababu binafsi, kuuza nyumba kunaweza kukuumiza kichwa sana. Hasa ikiwa una muda mdogo.

Ugumu unaweza kuongezeka zaidi ikiwa unaishi mikoa kama Dar es Salaam, Arusha au Mwanza ambapo kuna nyumba nyingi zinauzwa na wanunuzi ni wachache.

Mara nyingi wauzaji wa nyumba hukata tamaa hadi wanaishia kuuza nyumba zao kwa bei ya chini kuliko vile walivyotaka.

Kwa bahati nzuri, kuna mambo kadhaa unayoweza kufanya kukusaidia kuuza nyumba yako haraka bila kuathiri faida utakayotegemea kuitengeneza.

Hatua ya 1: Maandalizi

1. Linganisha Bei na Thamani

kuuza nyumba

Wauzaji wengi hukosea hapa. Wauzaji wengi wa nyumba huwa na dhana potofu kuwa, ni bora kuweka bei ya juu sana ya nyumba ili mnunuzi akija kutaka kununua watashushana mpaka kwenye mnunuzi anayotaka. Matokeo yake nyumba inabaki sokoni kwa muda mrefu kwani wanunuzi hawatajisumbui hata kuulizia.

Kuweka kiasi kikubwa cha fedha kuliko thamani halisi ya nyumba utafukuza wateja wengi, hasa wale waliofanya vizuri tafiti ya bei za nyumba kwa wakati huo. Na usipokuwa makini, utaishia kuwapa faida wauzaji wengine, kwani wateja wote watakimbilia kwenye nyumba zenye bei sahihi.

Mara zote, fanya tafiti ya bei za nyumba kabla ya kuweka yako sokoni. Angalia yako ina nini ya kuiongezea thamani, tuseme uwanja mkubwa zaidi, bwawa la kuogelea n.k. Mnunuzi ni lazima aone bei inavyoendana na thamani halisi

2. Andaa Nyumba Yako

Ni kama wakati unaenda kwenye usaili wa kazi. Muonekano wako wa kwanza ni muhimu sana. Hivyo hivyo kwa wanunuzi wa nyumba yako, bila kuikuta na mwonekano mzuri mara ya kwanza, wanaweza ata wasiulizie bei, wakaishia kuangalia na kuondoka. Hivyo ni muhimu kuhakikisha:

  • Unasafisha sehemu zote za ndani na nje ya nyumba.
  • Ikiwa rangi ni ya zamani na imepauka, paka mpya na nzuri
  • Ikiwa una bustani, hakikisha imepaliliwa na inahifadhiwa vizuri
  • Punguza vitu vinavyochukua nafasi kubwa ndani, vile vinavyofanya nyumba ionekane ndogo hata kama ina nafasi ya kutosha.

3. Fanya Wanunuzi Wajione Wako Nyumbani

Usiwe mbinafsi sana wakati wa uuzaji wa nyumba. Ili kusaidia wanunuzi waweze kujiona wanaweza kuishi nyumbani kwako (kama watanunua), basi huna budi kuondoa vitu vyote vya kibinafsi kama picha za familia,vitu vya kidini, vitu vya siasa, na sanaa za kipekee. Kuna baadhi ya wanunuzi wanaweza kuja nyumbani kwako lakini kutokana na kuona baadhi ya vitu fulani, mfano vya kudini basi wakashindwa kuvutiwa.

Fanya nyumba yako iwe sehemu isiyoegemea upande wowote na waachie wanunuzi waweze kujichorea kichwani maisha yao yatakavyokuwa kama wakiinunua.

Hatua ya 2: Kuuza

4. Tangaza kupitia Sehemu Tofauti Tofauti

kuuza nyumba

Ikiwa hautumii madalali ili wakusaidie kuuza nyumba yako, basi hakikisha unatangaza katika mitandao tofauti tofauti. Usitegemee tu kuwaambia watu kwa maneno ya mdomo au matangazo ya gazeti. Weka tangazo lako kwenye tovuti maarufu kama ZoomTanzania na mitandao ya kijamii: Facebook, Instagram.

Unaweza kujifunza jinsi ya kutangaza ZoomTanzania hapa

5. Kumbuka Picha Ndio Kila Kitu

Kumbuka, picha inazungumza maneno 1000. Hasa wakati wa kuuza vitu kama nyumba, wanunuzi wanavutiwa sana na kile wanachokiona katika picha. Kama huna utaalam wa kupiga picha, unaweza kuajiri wapiga picha wenye uzoefu. Piga picha kutoka pembe tofauti, nje na ndani, maeneo muhimu n.k.

6. Usiuze Nyumba Tu!

Wakati wa kutangaza nyumba yako, wanunuzi huwa hawahitaji kujua kuhusu nyumba tu. Jiongeze na ongelea vitu vingi zaidi kama huduma za muhimu zinazopatikana karibu. Vitu kama:

  • Maeneo gani (shule, hospitali, migahawa, baa, vituo vya ununuzi) yako karibu na nyumba hiyo?
  • Je, ni vitu gani unavyopenda kuhusu eneo hilo?

Hatua ya 3: Uza

7. Patikana Kirahisi:

kuuza nyumba

Japokuwa hili linaweza kuingiliana na ratiba zako nyingine, mfano kazi n.k., ni muhimu kuhakikisaha unapatikana kirahisi. Au unaweza kuweka maelezo ya muda kwenye tangazo lako ili wanunuzi wajue unakuwa huru muda gani. . Epuka kuwafanya wanunuzi kutaka kutaka kuona nyumba lakini wewe umebanwa. Wengine wataona ni uzushi.

Ikiwa unakosa muda wa kufanya yote haya kutokana na kazi au biashara zako, basi unaweza kuajiri mawakala wa nyumba na viwanja au kuwaachia madalali wafanye kazi hivyo. Hawa wanajua soko lilipo na wanaweza kukuokoa muda mwingi na pesa.

Mustapha Mosha
Mustapha Ally is a Community Marketing Manager at Zoom Tanzania and BrighterMonday Tanzania. He loves digital marketing social media