Hatua Rahisi za Kuuza Gari Lako kwa Bei Sahihi na Kwa Usalama

  | 4 min read
0
Comments
2553
kuuza gari

Katika hatua fulani ya maisha, inaweza kufikia siku ukataka kuuza gari lako. Labda unahamia nchi nyingine, au unahitaji fedha ya ziada, au unataka kununua gari lingine zuri zaidi. Kuuza gari lako si rahisi kama unavyodhani. Inaweza kugharimu muda, nguvu zako na hata pesa.

Ni kawaida kutaka kuuza kwa haraka na kwa bei unayodhani inafaa. Kama muuzaji, inatakiwa ujue mnunuzi anataka kujua nini hasa, na kumpa taarifa hizo kabla hajapata usumbufu wa kuziulizia. Bei inayoendana na thamani ya gari pamoja na maelezo ya gari yaliyokamilika yanasaidia kupunguza muda wa kuliuza gari lako.

Wanunuzi wengiwa magari huhitaji uhakika wakati wa manunuzi, hasa pale wanaponunua gari lililotumika. Hivyo kama unataka kuuza gari lako moja kwa moja bila kutumia madalali, ni vyema kuhakikisha tangazo lako linajitosheleza na mnunuzi wako hana chochote cha kukuhofia.

1. Cheza na Bei

kuuza gari

Wanunuzi wengi wa magari yaliyotumika (secondhand cars) huwa wanajua vizuri bei za magari wanayotaka kabla hawajaingia sokoni. Hivyo ni rahisi sana wakapita tangazo la gari lako ikiwa watakuta umeweka bei kubwa tofauti na thamani ya gari lenyewe.. Sawa, gari lako linaweza kuwa na vikorombwezo vya ziada mfano vioo vya tinted, kiyoyozi n.k hiyo isiwe sababu ya kuweka bei kubwa isiyo na mashiko.

Kama unakusudia kuliuza kwa haraka, basi weka bei inayoendana na magari mengine kisha tumia hivyo vikorombwezo kama vivutio vya kuvutia wateja wanunue gari lako na si mengine. Mfano, mpo wauzaji watano wa Toyota Vitz na bei zinalandana lakini gari lako tu ndio lina kiyoyozi na magurudumu mapya, unadhani wateja wataenda kwa nani?

2. Toa Dili Nzuri

Kuna zaidi ya 80% ya wanunuzi wa magari mtandaoni, na asilimia kubwa wanaamini kuwa mtandao ni sehemu nzuri sana ya kupata taarifa za masoko ya magari na kununua magari yenyewe. Ili uweze kuuza gari lako kwa haraka, ni lazima uwe walipo wateja wako. Na kumbuka kuwa, ili kumuuzia mtu gari lililotumika unahitaji kumuhakikishia kwamba anapata dili zuri. Hivyo unapoweka tangazo lako mtandaoni ni muhimu lionekane kama ni dili nzuri. Kuanzia muonekano wa picha, maelezo yasiyopishana na picha, vikorombwezo, matairi mapya, bima iliyolipiwa, nakadhalika. Hivi vinaweza kuongeza thamani ya gari lako. Hakikisha pia tangazo lako lina kila taarifa mteja anayotaka kuijua. Tafiti zinaonesha kuwa wateja wengi wa magari yaliyotumika hupenda kujua historia ya gari (ajali, kurudiwa rangi, kubadilishwa injini n.k

3. Kuwa Makini wakati wa Kukutana na Wanunuzi

kuuza gari

Baada ya kutangaza gari lako, sasa ni wakati wa kukutana na wanunuzi. Kuuza gari lako kunaweza kuhitaji muda wako wa ziada wa kukutana na watu mbali mbali walioonesha nia. hakikisha umewachuja na umejiridhisha wanunuzi utakaotaka kukutana nao ili kuepuka usumbufu usio wa lazima.

Baada ya kukubaliana kukutana, hakikisha mnakutana sehemu ya wazi, mfano Mlimani City. Waoneshe gari, wakague kila kona ukiwepo. Jibu maswali yao kwa kadri unavyoweza na kabla hajalijaribu kwa kuliendesha, hakikisha kuwa ana leseni ya udereva. Kisha kaa upande wa abiria wakati anaendesha

4. Patana Bei

Kila mtu anataka bei nzuri. Hata kama kwenye tangazo uliweka wazi kabisa kuwa bei ya gari haina maongezi, baadhi ya wanunuzi watakufata na kutaka maongezi., inatakiwa uwe umejiandaa kwa hili. Baada ya kukagua gari na vitu vingine, unaweza kuulizwa “Kwa hiyo bei ya mwisho ngapi Boss?” Usishangae, kama uliainisha wazi kuwa bei haishuki basi weka wazi katika hilo. Lakini kama ulipanga kushusha kidogo, unaweza kumjibu kwa swali pia, kama vile “Wewe unatoa ngapi Boss?”. Mwache yeye ndio ataje bei kwanza, halafu wewe ndio uangalie kama utaridhika au vipi. Usije kutaja bei wewe, ukakuta alikua amepanga kulipia kubwa zaidi. Kupatana bei wakati mwingine ni sanaa, inahitaji ujanja fulani.

5. Kamilisha Mauzo ya Gari Lako

kuuza gari

Mkishakubaliana bei na siku ya makabidhiano, kuna vitu utahitaji kabla ya kuhamisha umiliki wa gari lako kwa mtu mwingine. Mauzo ya gari ni tofauti kidogo na mauzo ya vitu kama TV au simu. Hayawezi kukamilika bila uhamisho wa hati miliki. Pia kuna haja ya kuwepo mashahidi na mwanasheria ili mauziano yawe halali. Usisahau kuweka vitu kama rekodi za matengenezo ya gari au makaratasi mengine muhimu yanayoweza kuhitajika kisheria. Baada ya hapo unaweza kukabidhi funguo ya gari.

Mustapha Mosha
Mustapha Ally is a Community Marketing Manager at Zoom Tanzania and BrighterMonday Tanzania. He loves digital marketing social media