Mambo 5 Muhimu ya Kuzingatia Kabla ya Kupanga Nyumba

  | 3 min read
0
Comments
5878
kupanga nyumba

Wengi tunaweza kupitia hili  — umeona nyumba mtandaoni, umeipenda  sana hadi unavuta picha kichwani kwako ukiishi humo. Hii inakuja baada ya kuhangaika sana kutafuta nyumba, na hii ulioiona inakua  nzuri kuliko zote, hivyo hauna namna. Na wakati mwingine kama unatumia dalali, anaweza kukwambia kuna watu wanataka kuilipia hivyo ufanye hima sana kabla hujaikosa. Kabla ya kuingia mfukoni na kukamilisha mambo, ni muhimu kukaa, kukagua vitu vingi kuhusiana na nyumba hiyo kabla ya kuja kujuta wiki moja baada ya kuhamia.

Hivi ni baadhi ya vitu muhimu unapaswa kuvizingatia kabla ya kupanga nyumba unayotaka kuhamia.

  1. Eneo Nyumba ilipo na Umbali

kupanga nyumba angalia eneo

Inaweza kuwa nyumba nzuri sana kwa muonekana , lakini kama itakufanya utumie masaa mawili njiani au kuongeza gharama za usafiri, basi fikiria mara mbili. Kila mara  anza kwa kuangalia usafiri wako, usafiri wa umma, foleni pamoja na uwezekano wa kufika baadhi ya maeneo muhimu. Inachosha kama itakubidi kila siku uamke masaa mawili mapema zaidi ili tu uwahi kwenda kazini, na siku hali ya hewa ikiwa mbaya kidogo basi unachelewa.

Ukiachana na usafiri, eneo hilo ni salama? Kama marafiki zako hawawezi kuja kukutembelea mida ya jioni kuhofia kukabwa, basi ni wazi hilo ni eneo la kuwa muangalifu nalo.

  1. Marekebisho

Kabla ya kupanga nyumba, pia fikiria kuhusu marekebisho utakayotakiwa kuyafanya wakati wa kuhamia. Kuna baadhi ya nyumba zinakua zinaonekana vizuri tu kwa nje. Lakini ndani, marekebisho yanakuwa makubwa na huweza kukuongezea gharama zisizo za msingi. Wapangaji watakaokuwa wamehama katika nyumba hiyo wanaweza kuwa wameacha nyumba katika hali ambayo wewe huwezi kuishi bila kuirekebisha. Mfano, mfumo wa maji safi na maji taka, umeme n.k. Baadhi ya wamiliki wa nyumba hufanya marekebisho thabiti kwa gharama zao kabla ya kuruhusu wapangaji wapya kuhamia. Hivyo kuwa makini na kujadiliana na mwenye nyumba juu ya gharama na marekebisho.

  1. Makatazo ya Nyumba yanaendana na Mahitaji Yako?

kupanga nyumba makatazo ya nyumba

Wakati mwingine, kabla ya kufikia makubaliano ya kupanga nyumba, mwenye nyumba anaweza kukaa  nawe kujadili machache kuhusiana na namna utakavyoishi katika nyumba yake. Wakati wa kupanga, hakikisha unajua kwa makini kuhusu nyumba hiyo na sheria zake  kwa ujumla. Baadhi ya nyumba zina makatazo fulani kuhusu vitu kama kikomo cha sauti za redio, matumizi ya maji, uchomaji taka, michezo ya watoto n.k. Hakikisha unajua vyote hivi kabla ya kufanya malipo.

  1. Gharama za Ziada Zikoje?

Wakati mwingine, gharama za kupanga nyumba zinajumuisha gharama nyingine za ziada. Kwa baadhi ya nyumba, wapangaji hushea gharama za umeme na maji. Gharama kama hizi zinaweza kutofautiana kutokana na sababu tofauti, mfano, ukubwa wa nyumba yako pamoja na matumizi yake. Hivyo kabla ya kuhamia, hakikisha unajua nyumba unayoamia gharama za ziada zinaingia vipi? Kama matumizi ya umeme wa LUKU na maji ni yako peke yako au mnachangia  na wapangaji wengine. Na kama ni wa kuchangia , basi uwiano wake unakuwaje kulingana na ukubwa na matumizi yako na yao.

  1. Soma Mkataba Kwa Makini

kupanga nyumba soma mkataba kwa makini

Wengi wetu hufikiri ukishalipa kodi basi  hakuna kinachoweza kwenda kombo. Lakini mambo yanaweza kubadilika kama usipokuwa makini. Kama ambavyo unakubali kwa kuandika kuwa utalipa kodi kwa wakati na kuitunza nyumba vyema, hakikisha unasoma  mkataba wako unaorodhesha/ majukumu ya mwenye nyumba yako kwa kipindi utakapokuwa unaishi hapo. Hii inajumuisha marekebisho na mambo anayotakiwa kukusaidia endapo utahitaji. Soma mkataba vizuri na hakikisha unaelewa na kuomba msisitizo sehemu ambayo haieleweki. Ni vema zaidi kuongea na mwanasheria ambaye anaweza kukusaidia kutafsiri kwani mikataba mingi Tanzania inaandikwa kwa Kiingereza.

Mustapha Mosha
Mustapha Ally is a Community Marketing Manager at Zoom Tanzania and BrighterMonday Tanzania. He loves digital marketing social media