Njia 5 za Kuendesha Gari kwa Usalama Msimu wa Mvua

  | 3 min read
0
Comments
4191
gari msimu wa mvua

Kuendesha gari wakati wa mvua huwa ni changamoto, na wakati mwingine si salama kabisa. Mara zote unapokua nyuma ya gurudumu wakati wa mvua kubwa, ni lazima uwe makini sana na uendeshaji wako. Tayari kuna mambo mengi yanayoweza kukupotezea umakini, na ukijumlisha mwonekano hafifu pamoja na barabara mbovu, kuna hatari kubwa ya kupata ajali. Kwa hiyo  ni bora kuchukua tahadhari mapema. Hizi ni baadhi ya namna za kuendesha gari wakati wa mvua ili kupunguza hatari ya ajali.

1. Fikiria Kwanza Kuhusu Mwendo!

gari msimu wa mvua punguza mwendo

Hili ni wazi na linaeleweka kabisa. Vibao vya kuongoza mwendokasi barabarani vimewekwa kwa matumizi ya msimu ambao si wa mvua;  msimu unapoendesha ukiona na hali ya hewa iko shwari. Lakini ni tofauti kukiwa na mvua. Mwonekano wa barabara ni hafifu na maji yanasababisha matairi ya gari kuteleza na kumpa wakati mgumu dereva kuliongoza gari. Jaribu kupunguza mwendo, hata kama kibao kinaonesha ni 50Km/s. Jaribu kwenda chini ya hapo na utafika kwa usalama zaidi.

2. Hakikisha Vioo Havina Ukungu na ni Visafi

Mwonekano mzuri ni muhimu sana wakati wa kuendesha gari, hasa msimu wa mvua. Ni muhimu sana kuhakikisha vioo vya gari lako havina aina yeyote ya uchafu, tope, unyevu au ukungu wakati unaendesha. Kama kioo cha gari lako kina hitilafu yeyote inayokuzuia kuona vizuri, basi rekebisha mapema kabla msimu wa mvua haujaanza. Na katika matumizi ya vifuta maji (windowscreen wipers) za kioo cha mbele na nyumba, hakikisha zinasafisha vyema ama ubadilishe mapema. Vifaa vingi vya magari vinapatikana mitandaoni, unaweza kuagiza au kuita fundi wakufungie.

3. Jihadhari na Kuserereka

gari msimu wa mvua jihadhari na kuserereka

Kuserereka kwa gari (hydroplaning) hutokea pale ambapo matairi ya gari yanashindwa kushikamana vyema na barabara hivyo kushindwa kuliongoza gari lako. Mara nyingi hutokea pale unaposhika breki za ghafla wakati ukiwa kwenye kasi kubwa. Kuzuia gari lako kutoserereka wakati wa mvua, hakikisha unaenda mwendo wa wastani na pia lipe gari la mbele yako umbali wa kutosha ikiwa dharura itatokea uweze kumudu vyema. Pia, itasaidia sana kukagua magurudumu ya gari lako kabla ya msimu wa mvua. Kama yana kipara basi yabadilishe.

4. Kuwa Makini na Madimbwi ya Maji Yaliyotuama

Wakati wa mvua kubwa, si tu unaweza kuathirika na mserereko wa gari, bali unaweza kuharibu gari lako ama kuvunja springi (Suspensions) kama utapita kwa kasi juu ya madimbwi yaliyojaa maji. Pia  unaweza ukawamwagia maji watumiaji wengine wa barabara. Hili linaweza kusababisha ajali maana wanaweza kupoteza mwelekeo na kuingia barabarani.

5. Usiache Kuwasha Taa za Mbele

gari msimu wa mvua usiache kuwasha taa za mbele

Sheria inaruhusu matumizi ya taa za mbele wakati wa mvua au uonaji hafifu barabarani. Mvua zinaweza zikapunguza uwezo wa kuona mbali ukiwa ndani ya gari na kukupa changamoto ya kupishana kwa usalama na madereva wengine. Hivyo ili uwe katika usalama zaidi, ni vyema ukawasha  taa zako ili kuwatumiaji wa barabara walio mbela na nyumba yako waweze kukuona.

Mustapha Mosha
Mustapha Ally is a Community Marketing Manager at Zoom Tanzania and BrighterMonday Tanzania. He loves digital marketing social media