Hatua 7 Rahisi za Kuanzisha Bustani Nyumbani Kwako

  | 3 min read
0
Comments
8146
bustani nyumbani

Bustani ya nyumbani ni hobi inayoweza kuliwaza na kuvutia. Inakupa muda mzuri wa kufanya mazoezi ya ziada na pia kukutanisha familia pamoja. Kuwa na bustani ndogo nje ya nyumba ni kazi inayoweza kukupa utulivu na kukufurahisha sana. Ukiacha sababu ya kuwa kama pambo la nyumbani, bustani zina faida nyingi.

Wengi huamua kuweka kama sehemu ya kupanda dawa za asili, mfano Mshubiri (Aloe Vera), isiyopatikana kirahisi baadhi ya mikoa. Wengine hutumia kama sehemu ya kupanda viungo, mfano michaichai n.k, na wengine huwa na bustani isiyo na maua, aghalabu bustani ya ukoka kama uwanja wa watoto kujifurahisha. Ikiwa umepanga kuwa na bustani ya nyumbani, kutokana na sababu yeyote ile basi hujachelewa. Hizi ni hatua rahisi za kuanzisha bustani nyumbani

  1. Anza Kidogo

bustani nyumbani

Hatua ya kwanza kabisa ya kitu chochote ni kuanza. Usisumbuke na swali la wapi utaanzishia bustani yako. Unaweza kupanda mbegu ama miche michanga kwenye vikopo (containers). Hii ni njia ya kukuza taratibu miche ama mbegu. Hakikisha vikopo vimewekewa udongo mzuri wenye  mchanganyiko wa mbolea kidogo karibu na nyumba, ambapo unaweza ukavitanzama kwa urahisi. Ukuaji wa miche yako utakuwezesha kupata picha halisi ya wapi hasa mimea yako itafaa kukaa

  1. Hakikisha Kuna Udongo Mzuri na Wenye Rutuba

Udongo wa vikopo au eneo utakalopanda miche yako unatakiwa kuwa na rutuba ya kutosha na mfumo mzuri wa maji.. Changanya udongo na mbolea asili. Kwa watunza bustani wazuri, mbolea ya asili si shida sana kupata. Unaweza kutumia mabaki ya vyakula kama  maganda ya matunda ama mbolea ya kuku ama ngombe. Unaweza kutumia mbolea mbadala, ingawa mbolea ya asili ni nzuri zaidi.

  1. Eneo Ndio Kila Kitu

bustani nyumbani eneo ndio kila kitu

Unapofikiria eneo la bustani yako, haitakiwi ufikirie kwa mwonekano wako wewe. Kwamba wapi ikikaa ndio itapendeza. Kila mimea inatofautiana. Kuna ambayo inahitaji jua kwa wingi, na mingine inahitaji kivuli . Na baadhi ya mimea inahitaji vyote. Hivyo ni vizuri kuzingatia eneo na hali ya hewa. Ukiweza kupangilia hivi, basi hutakuwa na kazi kubwa sana katika kuhakikisha unapata matokeo chanya katika bustani yako uliyoianzisha .

  1. Zingatia Aina na Nyakati

Kupata matokeo mazuri katika upandaji maua kwenye bustani yako, unahitaji kupanda maua sahihi katika msimu sahihi. Kwa nchi kama Tanzania, mikoa tofauti ina hali za hewa tofauti. Mfano joto la Dar es Salaam na baridi ya Iringa au Mbeya. Hivi vyote vinaathiri ukuaji wa baadhi ya mimea . Zingatia pia tabia za hali ya nchi , kwa mfano; hapa kwetu mwezi Disemba hadi February ni miezi ya joto na jua kali, wakati miezi ya Machi hadi Mei ni miezi ya masika. Hivyo ni muhimu kuzingatia aina ya mimea unayotaka kuanza nayo kulingana na kipindi cha msimu uliopo.

bustani nyumbani zingatia nyakati

Ingawa maua yana stahimili misimu ya hali ya hewa, mengi yanastawi vizuri zaidi kipindi cha mvua.  Pia yapo yanayo stawi katika kiangazi na masika mfano maua kama Acashia, Allium, Alstromeria, Asiatic, Lily na  Rose.

  1. Palilia, Ipe Bustani Yako Uhai

Hakikisha unaondoa magugu na vioteo vingine kwenye bustani ili kuifanya kuwa  na muonekano safi na wakuvutia. Hudumia bustani yako kwa ku palilia kila baada ya muda na fyeka majani marefu. Hii pia itasaidia kuboresha mzunguko wa maji, hewa na chakula kwenye maua au mazao yako na kuyapa muonekano mzuri na safi.

  1. Achana na Madawa, Fanya iwe ya Asili.

bustani nyumbani mbolea asili

Kuzingatia njia za asili kuhudumia bustani yako ni bora zaidi. Hakuna haja ya kuwa na bustani nzuri ya nyumbani ikiwa unatumia kemikali zinazoweza kuhatarisha usalama wa afya yako. Kwa mfano unaweza kutumia mbolea silia, na dawa za asili za kuzuia wadudu. Kemikali na mbolea mbadala zinaweza kukupa matokeo hasi na hata kunyausha maua yasipo zingatiwa. Fuatilia njia bora za asili za kutunza bustani kwa wataalamu.

Mustapha Mosha
Mustapha Ally is a Community Marketing Manager at Zoom Tanzania and BrighterMonday Tanzania. He loves digital marketing social media