Njia 6 za Kuboresha Tangazo Lako La Zoom Tanzania

  | 4 min read
0
Comments
1310

Kuuza ni zaidi ya kuweka tangazo lako kwenye mtandao wa Zoom Tanzania. Unaweza kuweka na usifanikiwe kuuza. Hii itakuja kama hautozingatia mambo muhimu yanayoweza kukupa wateja, kama jinsi unavyoliweka tangazo lako, namna unavyofuatilia wateja wanaonesha kuihitaji bidhaa yako, nakadhalika. Mambo haya ni muhimu sana sio kwa wauzaji wapya tu, bali hata wale ambao wamekuwa wakiuza kwa muda. Teknolojia inabadilika na ni muhimu kwa kila muuzaji, haijalishi kama ni mdogo ama mkubwa, mpya ama wazamani, kuwa na mkakati endelevu wa kwenda na muda katika uuzaji wa bidhaa na huduma kwenye mitandao kama mtandao wa Zoom Tanzania. 

Embu, tuangalie mambo machache ambayo yanaweza kukusaidia kuuza kwa urahisi na haraka. 

  1. Hakikisha Tangazo Lina Maelezo Yote

1.pngUkiweka tangazo lako kwenye tovuti ya Zoom Tanzania, hakikisha unatoa maelezo yote yanayohitajika. Hili litamsaidia mnunuzi kuweza kufanya maamuzi sahihi. Pia, itapunguza muda wa kuulizana maswali mengi kwa maana kila kitu kitakuwa kimewekwa wazi. Kama ni simu, hakikisha unaweka hali yake (condition), bei yake, na kama imetumika Tanzania ama nje ya nchi. Ongelea “specifications” zake na kama unaweza kusafirisha ama vipi. Kutoa maelezo ya kutosha kutakusaidia uweze kuuza haraka kwa maana wateja wanapenda kununua vitu ambavyo vimeelezewa vizuri. Usisahau kujitofautisha na wauzaji wengine ambao hawatilii maanani utoaji wa maelezo kuhusu bidhaa zao.

2. Picha Nzuri Huuza, Mbaya Hukimbiza Wateja

2.pngUkishapiga picha ya bidhaa ama kitu unachokiuza, jiulize je wewe kama ungeiona picha hizo ungevutiwa nayo? Kuna wauzaji wapya na hata wa zamani ambao wanapiga picha ili mradi wakamilishe mchakato wa kuweka tangazo lao. Usifanye hivyo kwa maana hautafanikiwa kuuza bidhaa ama kitu chako. Weka picha zenye sifa hizi

  • Zilizo angavu. Usipige kwenye giza ama sehemu isiyo na mwanga vizuri. Hakikisha picha zinaonesha bidhaa vizuri na kwa uhalisia wake.  
  • Picha zisiwe zimetingishika. Tuliza mkono ama kama huwezi tafuta mtu mwenye mkono usiotingishika.
  • Zinazoonesha bidhaa yako kwenye pande tofauti. Kama ni simu basi piga mbele na nyuma. Kama ni gari basi hakikisha una picha zinazolionesha mbele, nyuma, ndani, kwenye injini na hata kwenye buti.

3. Lugha Tamu Itakusaidia Kuuza 

Hakikisha lugha unayotumia na hata sauti yako wakati wa kuongea na mnunuzi ni yenye mvuto. Jiulize, je mimi ningependa kama muuzaji angeongea na mimi hivi? Kama hapana, basi badilisha jinsi unavyoongea na mteja. Hata kama mteja anauliza maswali ambayo unaona ni ya kijinga, usimuonesha kuwa huna muda wa kumsikiliza. Hata kama ana maswali mengi usichoke kujibu kwa ufasaha na kwa sauti nzuri. Wahenga walisema, mteja ni mfalme. Ikiwa umepigiwa na mteja na uko sehemu ambayo huwezi kuzungumza, mjulishe kuwa unatampigia baadae. Kama amekutumia meseji kwa WhatsApp basi andika meseji kwa ufasaha na isome kabla haujaituma. Kama kuna picha zaidi ambazo unaweza kumtumia, fanya hivyo. Jaribu kumuuliza mnunuzi ni kitu gani anahitaji ili umpe huduma ya kuridhisha. 

4. Jiongeze

Jiongeze ili uwe muuzaji mzuri. Kama kweli unataka kuipata hiyo elfu thelathini ya kiatu unachouza, ama hiyo elfu ishirini na tano ya fulana unayotaka kuiuza basi jiongeze. Ina maana gani pale mtu anaposema jiongeze? Embu tuangalie mifano michache. 

  • Mteja akiktumia meseji, mpigie simu kuonesha uko tayari kwa biashara. 
  • Mteja akikutumia email ama meseji, usipoteze muda kabla ya kumjibu. Mjibu mapema kwa maana anaweza kununua bidhaa ya muuzaji mwingine. 
  • Mpe mteja njia tofauti za kumfikishia bidhaa. Usiseme, mie nauza, usafiri utajijua mwenyewe. Hata kama hutoi usafiri, mpe njia mbadala za kukufikia. Je ni mabasi gani yanafika hapo? Je mnaweza kukutana wapi ambapo patakuwa karibu naye ili kufanya biashara. 

Usimfanye mteja akutafute. Jiongeze!

5. Ondoa Tangazo unapouza bidhaa yako

Kama unauza bidhaa tofauti, basi hakikisha kuwa unazitoa zile unazoziuza kutoka kwenye tovuti. Sio jambo zuri kuacha tangazo la bidhaa ambazo hunazo tena. Kwanza, inamuonesha mnunuzi kwamba hauko makini na biashara yako kwa kushindwa kusimamia orodha ya matangazo yako. Pili, inampotezea muda na fedha mnunuzi kwa kupiga simu na kuulizia bidhaa ambayo haipo tena. Athari ya hili ni kwamba kuna uwezekano mkubwa sana kuwa mnunuzi ataacha kuwasiliana na wewe akiamini kuwa bidhaa zako zote utakuwa umeshaziuza. 

6. Jifunze kwa Kuangalia Matangazo ya Wauzaji Wengine

6.pngJifunze kutoka kwa wauzaji wengine kwa kuangalia ni jinsi gani wanatangaza bidhaa zao. Angalia mambo makubwa mawili. Kwanza angalia ni mambo gani wanayofanya vizuri ambayo wewe huyafanyi. Kisha yawekee mkakati wa kuyaingiza katika mfumo wako wa uuzaji. Pili, jifunze na mambo gani ambayo hawayafanyi vizuri na uyaepuke. Tembelea mitandao zaidi ya Zoom Tanzania ili ujifunze zaidi. Itakuwa vema zaidi kama utajifunza kutoka kwa wauzaji walio nje ya nchi pia.

Tumeona ni njia gani ambazo unaweza kuzitumia kuhakikisha una tangazo zuri na litakalovutia wanunuzi. Jiongeze kwa kusoma na kujadiliana na wauzaji wengine hasa pale unapopata changamoto ya kuuza kitu chako. Waulize ni kitu gani ambacho hawapendi katika tangazo lako. Lakini pia, jua kuwa unaweza kuwasiliana na timu iliyopo Zoom Tanzania kwa maana inaweza kukusaidia kuboresha tangazo lako. Timu nzima iko hapa kwa ajili yako na mafanikio ya Zoom Tanzania ni wewe kufanikiwa kuuza vitu vyako. Kama haujafungua akaunti, ingia leo ufungue na uanze kuuza. 

Stephen Swai
Stephen Swai is a Marketing Manager with a passion for using words to inspire, educate and transform.